Jumanne, 26 Novemba 2013

MTANZANIA HUYU ANAISHI KWA MATESO NA RISASI KICHWANI...



UJAMBAZI ni unyama, anayejishughulisha na kazi huyo ni mtu mbaya kupita kiasi. Hana stahili hata chembe ya kujumuika na jamii yenye raia wema.

Jambazi anaweza kubadili jina la mtu na kuitwa marehemu ndani ya kipindi cha kufumba na kufumbua. Leo hii, msomi wa sheria aliyebobea katika masuala ya katiba, Dk. Sengondo Mvungi, hayupo tena nasi hapa duniani. Majambazi wamekatisha uhai wake.

Dk. Mvungi alikuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na alipania kutumia elimu yake kuisaidia nchi kupata katiba bora sana. Ndoto yake imekatizwa, Mungu amlaze mahali pema peponi ila kwa hakika tuwaalani majambazi na tumuombe Mungu awafanye washindwe.

Ubaya wa majambazi anaujua vizuri sana Fredrick Mdima, ukimsikiliza, simulizi yake inatia huzuni mno. Maisha yake yamebadilika kabisa. 

Ana siku 134 akiwa anaishi na risasi kichwani. Madaktari wamejitahidi kuitoa imeshindikana, sasa amebaki mgonjwa, kila siku maumivu ya kichwa hayamuishi, kikohozi mara kwa mara. Anatia huruma sana.

Mpaka Julai 15, mwaka huu, Mdima alikuwa mzima kabisa. Akiwa katika harakati za maisha, alipanda Basi la RS, akitokea Kagera alikokwenda kwa shughuli zake za mihangaiko ya kusaka riziki, akawa anarudi Dar es Salaam ambako ndipo yalipo makazi yake.

TUJUE MKASA WAKE KAMILI

Mwandishi wetu alimtembelea Mdima, nyumbani kwake, Yombo Dovya, Temeke, Dar es Salaam, kwa hakika hivi sasa anaishi kwa shida, mwenyewe anasimulia:

“Nilipanda basi Muleba, Kagera, nikiwa na matumaini tele ya kufika Dar es Salaam salama. Ilikuwa saa 12:00 asubuhi, sikujua kama saa mbili zijazo maisha yangu yatabadilika na kuwa ya mateso.
“Saa 2:00 asubuhi, basi likiwa kwenye Kijiji cha Kasindangwa, tulikuta lori limepaki katikati ya barabarani, dereva wetu na kila abiria aliyeshuhudia, alidhani lile lori ni bovu. Tulikuwa watulivu bila wasiwasi wowote.

“Dereva wa basi akaamua kupita pembeni kwa kujibana, kumbe lile lori lilikuwa mtego. Ghafla majambazi zaidi ya 10 wenye silaha za moto, walilizunguka basi tulilokuwa tumepanda.
“Binafsi nilikuwa nimefuatana na mwanangu, Method mwenye umri wa miaka 16, kwa maana hiyo masahibu haya yalinikuta mwanangu akinishuhudia.

“Wale majambazi baada ya kuzingira letu, walimuamuru dereva alizime kabisa. Mmoja wao akasema kwamba kati yetu sisi abiria kuna mwenye bunduki, hivyo walimtaka awakabidhi.

 Kumbe walimlenga askari polisi aliyevaa kiraia ambaye alisindikiza basi letu na kukabiliana na wahalifu.

“Askari huyo hakujitokeza, wale majambazi wakaanza kumimina risasi ovyo kwenye gari. Wote tukawa tumelala chini, huku kila mmoja akipiga kelele kwa namna alivyoweza kuomba msaada na kumtaja Mungu.

“Nilikuwa nimekaa siti za nyuma, bahati mbaya ikawa zaidi kwangu, maana katika zile risasi zilizopigwa, mbili ziliniingia kichwani.

“Damu zilitoka nyingi, wale mjambazi wakaamrisha abiria watoke nje. Yule askari baada ya kuona mimi navuja damu, aliisogeza bunduki jirani yangu kisha yeye akashuka kama raia wa kawaida.

“Wale abiria walipokuwa wanatoka nje walikaguliwa na kunyang’anywa fedha, simu na mali nyingine. Baada ya kumaliza uporaji, wale majambazi waliingia ndani ya gari na kunikuta nimezungukwa na dimbwi la damu, wakajua nimeshakufa, kwa hiyo walichukua ile bunduki na kuondoka zao.

“Kuanzia hapo sikujua kilichokuwa kinaendelea, nilipata fahamu ikiwa saa 8.00 mchana nikiwa Hospitali ya Biharamulo kabla ya kuhamishiwa Bugando siku iliyofuata, yaani Julai 16.

“Pale Biharamulo madaktari waliweza kunitoa risasi moja tu, nilipopelekwa Bugando kulikuwa na matumaini ya kutolewa iliyosalia lakini nako ilishindikana. Nilihamishiwa Muhimbili ambako pia madaktari walisema haiwezekani kuitoa. Wakasema inabidi nikubali matokeo na niishi nayo kwa miasha yangu yote.

MATESO YAKE

Mdima sasa hana uwezo wa kuzungumza vizuri, maana risasi kukwama kwake kichwani, imesababisha uharibifu wa mfumo wa fahamu.

Anasema akiwa amezingirwa na sikitiko: “Risasi hii kichwani imenisababishia matatizo makubwa kiafya, ikiwa ni pamoja na kukohoa mara kwa mara, kuumwa kichwa na kutoongea vizuri.”

Anabainisha kuwa risasi hiyo ndani ya kichwa chake ni ulemavu mkubwa, maana kwa sasa muda mwingi anajiuguza kutokana na kusumbuliwa na maumivu makali mara kwa mara, hivyo kumfanya ashindwe kujishughulisha na harakati za kusaka riziki.

Anaeleza: “Kwa kawaida shughuli zangu ni ufundi na uuzaji wa spea za magari ila kwa sasa mtaji umekata. Sina fedha, tangu siku nilipopata janga la kupigwa risasi, sijaweza kujishughulisha ufundi wala uuzaji was pea, nipo tu najiuguza. Mimi na kuumwa, kuumwa na mimi.”

KILIO CHAKE

“Natamani sana apatikane daktari wa kuweza kuitoa hii risasi, natamani sana kurudi katika yake ya kawaida, niendelee na shughuli zangu niweze kuilea familia yangu, niwasomeshe watoto wangu,” anasema Mdima na kuongeza.

UNAWEZA KUMSAIDIA MDIMA

Mbali na ombi hilo la kutolewa risasi, Mdima anatoa wito kwa kila mwenye uwezo kumuwezesha kadiri anavyoweza aweze kuihudumia familia yake, maana yeye kama baba ambaye ndiye nguzo ametetereka na nyumba nzima imeyumba.

Kwa mtu yeyote aliyeguswa na kilio cha Mtanzania huyu, anaweza kuwasiliana naye kupitia simu nambari 0719 754770 au 0689 715277.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni